KANISA ANGLIKANA TANZANIA
DAYOSISI YA SHINYANGA
IBADA YA KUMWEKA WAKFU
ASKOFU WA PILI WA SHINYANGA
REV. CAN. CAPT. JOHNSON JAPHETH CHINYONG’OLE
KANISA KUU LA MTAKATIFU STEFANO, SHINYANGA
Wazo kuu: “Lisha Kondoo Zangu”
Jumapili ya 2 baada ya Ufunuo
14 Januari 2018
SEHEMU YA KWANZA
MATAYARISHO
Maelezo muhimu ya Awali:
Baadhi ya wageni waalikwa wataoneshwa mahali pa kuketi ndani ya kanisa mapema kabla ya ibada kuanza.Wageni waalikwa wengine na waumini wataketi katika mahema nje ya kanisa.
Makasisi/Wachungaji/Mapdre waingie kanisani na kuketi mahali pao mapema kabla ya Maaskofu.
Maandamano ya Maaskofu yatakuwa kama ifuatavyo: Maaskofu wajipange wawili wawili, wakitangulia Maaskofu wa Madhehebu au Makanisa Mengine. Kisha watafuata Maaskofu Wastaafu wa Kanisa Anglikana. Ndipo wafuate Maaskofu wa Madayosisi (Diocesan Bishops) wa Kanisa Anglikana. Ndipo afuate Askofu Mlezi WA Shinyanga, Kisha afuate Katibu Mkuu na Msajili wa Kanisa Anglikana Tanzania. Kisha Chaplain wa Askofu Mkuu, ndipo Askofu Mkuu awe wa mwisho.
Wimbo wa Maandamano: - (Nyimbo Standard 1)
Ikiongozwa na Kwaya ya UVUKE – DCT –Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu)
- Baba, Mwana, Roho, Mungu Mwenye enzi,
Kila tukiamka tunakuabudu.
Baba, Mwana, Roho, Mungu wa mapenzi,
Ewe Utatu tunakusifu.
- Baba, Mwana, Roho, wakuaminio,
Wanakutolea shukurani zao,
Wakusujudia malaika nao:
Wewe U mwanzo nawe U mwisho.
- Baba, Mwana, Roho, sisi tu gizani,
Utukufu wako haoni mkosa;
U Mtakatifu, nawe U mapenzi,
U peke yako, mwenzio huna.
- Baba, Mwana, Roho, Mungu Mwenye enzi,
Ulivyoviumba vyote vyakusifu:
Baba, Mwana, Roho, Mungu wa Mapenzi,
Ewe utatu, tunakusifu.
Mwanzo wa Ibada, Watu wakiwa wamesimama, Askofu Mkuu aseme yafuatayo:
Tumekusanyika hapa leo kwa tendo la kihistoria kwa waumini na wananchi wa Shinyanga la kumweka wakfu Johnson Japheth Chinyong’ole kuwa Askofu wa Pili wa Dayosisi ya Shinyanga. Kama wengine mnavyofahamu, Johnson Chinyong’ole amekuwa Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania kwa miaka mitatu. Johnson Chinyong’ole alichaguliwa mwezi Oktoba mwaka 2017kuwa Askofu wa Pili wa Shinyanga. Tunamwombea yeye na familia yake. Baadaye katika Ibada wenyeji watafanya utambulisho zaidi wa baadhi ya wageni. Lakini kwa sasa, na kipekee sana, napenda nitambue uwepo wa Mgeni wetu Rasmi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa. Karibu sana Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Ibada hii. Aidha nitambue pia uwepo wa Waheshimiwa Mawaziri waliopo, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Waheshimiwa Wabunge.
Kisha Liturgia ianze.
Askofu Mkuu: Kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
Wote: Amin
Askofu Mkuu asome Amri Kuu.
Bwana wetu Yesu Kristo alisema, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na Manabii.
Askofu Mkuu: Bwana Uturehemu.
Wote: Bwana Uturehemu
Askofu Mkuu: Kristo Uturehemu
Wote: Bwana Uturehemu
Askofu Mkuu: Bwana Uturehemu
Wote: Bwana Uturehemu
AskofuMkuu: Msaada wetu ni katika Jina la Bwana
Wote: Aliyeziumba mbingu na nchi
Askofu Mkuu: Wapendwa katika Bwana, tumuungamie Mungu dhambi zetu, kwa moyo mnyenyekevu uliotubu na kutii, ili tupate kusamehewa kwa wema na rehema zake zisizo na kikomo.
Hapa kabla ya maungamo uimbwe wimbo
Standard 107;
- Naweka Dhambi zangu,
Juu yake Bwana,
Kuziondoa kwangu,
Hulemea sana,
Na uaili wangu,
Ameuondoa,
Dawa yangu ni damu,
Kwa hiyo napoa.
- Na uhitaji wangu,
Nitamjuvisha,
Kwa upungufu wangu,
Yeye anatosha,
Majonzi yangu yote,
Na mizigo yangu,
Atachukua vyote,
Yesu Bwana wangu.
- Na roho yangu nayo,
Imechoka sana,
Namletea hiyo,
Ilindwe na Bwana,
Ni jema jina lake,
Nalo la pendeza,
IMANWELI; na kwake
- Natamani daima,
Niwe kama Bwana,
Mpole tena mwema,
Wa mapenzi sana,
Zaidi natamani,
Kwenda kwake juu,
Nikaone Mbinguni,
Enzi yake kuu.
Ungamo:
Mwenyezi Mungu, Baba wa Mbinguni, Twaungama kwamba tumekutenda dhambi wewe na jirani zetu, kwa mawazo, na maneno na matendo, na kwa kutotimiza yatupasayo.
Twasikitika sana,
Twatubu,
Kwa njia yake Yesu Kristo utusamehe
Na kutusafisha kwa Roho wako Mtakatifu,
Ili tuweze kukutumikia katika upya wa maisha, kwa Utukufu wa jina lako. Amin.
Askofu Mkuu asimame na atoe ghofira (tamko la msamaha wa Mungu kwa watu):
Mwenyezi Mungu anayewasamehe wote watubuo kwa kweli, akurehemuni, akusameheni dhambi zenu zote, akutieni nguvu, akuimarisheni katika wema wote. Akufikisheni kwenye uzima wa milele. Kwa Yesu Kristo Bwana wetu.
Wote: Amin
Watu wasimame na kusema UTUKUFU.
Askofu Mkuu aseme: Utukufu una Mungu juu mbinguni:
Wote: Amani duniani kwa watu aliowaridhia,
Twakusifu,
Twakuhimidi,
Twakuabudu,
Twakutukuza,
Twakushukuru
Kwa ajili ya utukufu wako mkuu,
Bwana Mungu
Mfalme wa mbinguni,
Mungu Baba Mwenyezi
Ee Bwana, Mwana pekee, Yesu Kristo
Bwana Mungu, Mwana Kondoo wa Mungu
Mwana wa Baba
Uichukuaye dhambi ya ulimwengu,
Uturehemu
Uichukuaye dhambi ya ulimwengu,
ukubali kuomba kwetu
Uketiye mkono wa kuume wa Mungu Baba,
uturehemu
Kwa kuwa ndiwe pekee yako Mtakatatifu,
ndiwe pekee yako Bwana
Ndiwe pekee yako uliye juu,
Yesu Kristo
Pamoja na Roho Mtakatifu,
katika utukufu wa Mungu Baba
Amin.
Askofu Mkuu: Bwana akae nanyi
Wote: Pia na roho yako.
Askofu Mkuu: TUOMBE
Mwenyezi Mungu, ambaye kwa Mwana wako Yesu Kristo uliwapa Mitume wako watakatifu karama nyingi zilizo bora, ukawaamuru walilishe kundi lako: twakusihi Maaskofu wote, Wachungaji wa Kanisa lako, walihubiri Neno lako kwa juhudi, na kuhudumia maadili yake matakatifu, uwajalie watu wako wayatii na kuyafuata ili wote waipokee taji ya utukufu wa milele. Kwa Yesu Kristo Bwana wetu.
Wote: Amin
Askofu Mkuu TUOMBE
Sala ya kuombea Kanisa na Dayosisi ya Shinyanga
Mwenyezi Mungu uishiye milele, uliyetufundisha tuombe na kutoa shukurani kwa ajili ya watu wote, Twakusihi kwa unyenyekevu ulivuvie daima Kanisa la ulimwenguni mwote roho ya kweli, na ya umoja; na hasa Dayosisi hii ya Shinyanga. Uwajalie wote wanaokiri Jina lako Takatifu, wapatane katika kweli ya Neno lako Takatifu na kuishi kwa umoja na upendano. Tunaleta maombi yetu haya kupitia kwa Yesu Kristo Bwana wetu.
Wote: Amin
Watu wakae.
WIMBO: KWAYA – Kwaya ya Kanisa Kuu
SOMO LA WARAKA. 1 TIMOTHEO 3:1-7
Somo lisomwe na Askofu Darlington Bendakheha wa Dayosisi ya Kagera
Msomaji aseme:
Sikilizeni Neno la Mungu, kama lilivyoandikwa katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Timotheo sura ya tatu, kuanzia aya ya kwanza hadi ya saba.
“Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya Askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa Askof u awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?. Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”
Ndilo Neno la Bwana
Wote: Tumshukuru Mungu
WIMBO: KWAYA
Watu wasimame.
SOMO LA INJILI. YOHANA 21: 15-17.
Somo lisomwe na Askofu James Almasi – Askofu wa Dayosisi ya Masasi
Msomaji aseme:
Sikilizeni Neno la Mungu kama lilivyoandikwa katika Injili kama alivyoiandika Yohana Mtakatifu, sura ya ishirini na moja kuanzia aya ya kumi na tano hadi aya ya kumi na saba.
Wote: Atukuzwe Bwana
“Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia tena mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.
Ndilo Neno la Bwana
Wote: Asifiwe Kristo
Nyimbo Standard 363
- Nipe moyo wenye sifa
Sio wa utumwa;
Damu ulionyunyizwa,
Wa kwimba daima.
- Moyo msikizi moyo,
Wa kunyenyekea,
Moyo utawaliwao,
Na Mwokozi pia.
- Wenye,kutubu,mnyonge
Sadiki, amini,
Kamwe,kamwe,asitengwe, Akaaye ndani.
- Mpya, mwema na mawazo,
Mwingi wa mapenzi,
Na uwe kielelezo
Moyo wa Mwokozi.
- Ni uule moyo wako;
Moyo wa huruma,
Yesu natamani kwako,
Kukujua vyema.
- Na ya midomo matunda,
Yako, nipe name;
Amani isiyokoma,
Iwe yangu mimi.
- Nitie yako tabia,
Inishukie juu;
Jina lako nipe pia,
Ndilo la Pendo tu.
- Ni wa Baba utukufu;
Mwana atukuke;
Na Roho Mtakatifu:
U Utatu pweke.
MAHUBIRI – Askofu Donald Mtetemela- Askofu Mkuu Mstaafu.
Baada ya Mahubiri Watu wote wasimame kusema IMANI YA NIKEA
Askofu Mkuu: Twamwamini Mungu mmoja,
Wote: Baba Mwenyezi. Muumba Mbingu na Nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana: Na Bwana mmoja Yesu Kristo Mwana pekee wa Mungu Mwana wa azali wa Baba Yu Mungu kutoka katika Mungu Yu Nuru kutoka katika Nuru Yu Mungu kweli: Mwana wa azali, asiyeumbwa mwenye Uungu mmoja na Baba: Kwa yeye huyu vitu vyote viliumbwa: Aliyeshuka kutoka Mbinguni kwa ajili yetu wanadamu na kwa wokovu wetu, Akatwaa mwili kwa Uweza wa Roho Mtakatifu, katika Bikira Mariamu, Akawa mwanadamu, Akasulubiwa kwa ajili yetu Zamani za Pontio Pilato, Aliteswa, akazikwa, Siku ya tatu akafufuka, Kama yenenavyo Maandiko Matakatifu, Akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Baba, naye atakuja tena kwa utukufu, kuwahukumu watu walio hai na wafu, na ufalme wake hauna mwisho. Twamwamini Roho Mtakatifu, Bwana mtoa uzima, atokaye katika Baba na Mwana, anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana, Aliyenena kwa vinywa vya Manabii, Twaamini Kanisa moja, Takatifu, Katholiko na Apostoliko, Twakiri ubatizo mmoja wa kuondolea dhambi, Twatazamia kufufuliwa kwa wafu, Na uzima wa ulimwengu ujao. Amin.
WATU WAKETI.
WIMBO wa Kwaya: UVUKE – Dodoma: Zaburi 139 ‘Ee Bwana Umenichunguza’.
SEHEMU YA PILI:
KUMWEKA WAKFU ASKOFU
Kwaya inapoimba, KITI CHA ASKOFU MKUU KILETWE mbele ya Meza Takatifu, naye Askofu Mkuu akae katika kiti chake. Maaskofu wawili walioandaliwa watafika mbele ya Askofu Mkuu, nao wainamishe vichwa vyao kama ishara ya kuomba idhini ya kumleta Askofu Mteule kwa Askofu Mkuu. Baada ya hapo waende mbele ya Askofu Mteule, nao watoe ishara ya kumtaka asimame. Askofu Mteule asimame. Maaskofu wamwongoze, mmoja akiwa mbela yake, na mwingine nyuma yake, waende wasimame mbele ya Askofu Mkuu.Askofu Mteule akiwa katikati, wote watatu wasimame mbele ya Askofu Mkuu, na kuinamisha vichwa vyao kutoa ishara ya kuomba idhini ya Askofu Mkuu kumpeleka Askofu Mteule kuvaa sehemu ya vazi la Kiaskofu, yaani Rochet. Kisha wataondoka, Askofu Mteule akiwa katikati.
Askofu Mteule akiwa amevaa rochet yake, aletwe na Maaskofu wawili kwa Askofu Mkuu.
Kisha Maaskofu wanaomleta Askofu Mteule waseme:
Baba mwenye heshima katika Mungu, Tumekuletea mtu huyu, Mcha Mungu, na mwenye elimu, aamriwe na kuwekwa wakfu kuwa Askofu.
Askofu Mkuu: Msajili wa Jimbo na asome Hati ya Kumweka Wakfu Askofu.
Askofu Mkuu aweke saini yake kwenye hati hiyo. Msajili wa Kanisa Anglikana Tanzania pia athibitishe kwa kuweka saini yake. Kisha Askofu Mteule Reverend Canon Capt. Johnson Japheth Chnyong’ole atatoa viapo vyake kama ifuatavyo.
Kiapo cha Utii kwa Askofu Mkuu
Katika jina la Mungu, Amin. Mimi Johnson Japheth Chinyong’ole, niliyechaguliwa kuwa Askofu wa Kanisa na Dayosisi ya Shinyanga nakubali na kuahidi kumheshimu na kumtii, kama inipasavyo, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania JACOB ERASTO CHIMELEDYA na watakaofuata baada yake; Mwenyezi Mungu anisaidie.
Kiapo hiki kimetolewa nami leo, siku ya Jumapili tarehe kumi na nne ya Mwezi wa Januari, katika mwaka wa Bwana wetu YESU KRISTO wa Elfu Mbili na Kumi Nane na kutiwa saini yangu.
Askofu Mteule aweke saini yake kwenye hati hiyo. Msajili wa Kanisa Anglikana Tanzania pia athibitishe kwa kuweka saini yake.
Kiapo cha Utii kwa Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania
Mimi, Johnson Japheth Chinyong’ole, niliyechaguliwa kuwa Askofu wa Kanisa na Dayosisi ya Shinyanga,
NINAAHIDI kwamba nitaifundisha na kuitii Imani ya Bwana wetu YESU KRISTO na Elimu ya Dini na Taratibu na Maadili na Marudi kama alivyoamuru kwa Kanisa lake, na kama ilivyokubaliwa na kuelekezwa na Kanisa Anglikana Tanzania katika Katiba ya Kanisa hili.
NINAAHIDI pia kwamba ninakubali kufungwa na Sheria na Kanuni zote zilizowekwa na zitakazowekwa tangu sasa na Sinodi ya Kanisa Anglikana Tanzania.
NINAAHIDI pia kwamba nitakubali kujiuzulu au kujitoa kwa hukumu yoyote itakayoniachisha madaraka na mapato yanayohusika na Dayosisi hii nitakayohukumiwa wakati wowote baada ya uchunguzi wa kutosha wa Baraza lenye kibali cha Sinodi ya Kanisa.
Kiapo hiki kimetolewa nami leo, siku ya Jumapili tarehe Kumi na Nne ya Mwezi wa Januari, katika mwaka wa Bwana wetu YESU KRISTO wa Elfu Mbili na Kumi Nane na kutiwa saini yangu..
Kiapo cha Utii kwa Katiba ya Dayosisi ya Shinyanga
Mimi, Johnson Japheth Chinyong’ole, niliyechaguliwa kuwa Askofu wa pili wa Dayosisi ya Shinyanga,
NINAAHIDI kwamba nitaiangalia misingi, sheria na kanuni za Dayosisi hii kama zitakavyoundwa mara kwa mara na Sinodi ya Dayosisi hii.
NINAAHIDI pia kwamba nitaitisha vikao vya Sinodi ya Dayosisi kwa nyakati za kawaida kadri itakavyotakiwa mara kwa mara kufuata maazimio ya Sinodi.
NINAAHIDI pia kwamba nitakubali kustaafu kazi nifikiapo umri wa miaka 65.
NINAAHIDI pia kwamba nitajiuzulu wakati wowote kama ikiazimiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa na ya Dayosisi hii. Mwenyezi Mungu anisaidie.
Kiapo hiki kimetolewa nami leo, siku ya Jumapili tarehe kumi na nne ya Mwezi wa Januari, katika mwaka wa Bwana wetu YESU KRISTO wa Elfu Mbili na Kumi Nane na kutiwa saini yangu.
Ndipo Askofu Mkuu asimame na kusema:
Ndugu, imeandikwa katika Injili ya Luka Mtakatifu, kwamba Mwokozi wetu Yesu Kristo alikesha usiku kucha akiomba, kabla ya kuwachagua na kuwatuma Mitume wake kumi na wawili. Imeandikwa tena katika matendo ya Mitume, kwamba wanafunzi waliokuwako Antiokia walifunga na kuomba, kabla ya kuwawekea mikono Paulo na Barnaba, na kuwatuma, basi na sisi, tukifuata mfano wa Mwokozi wetu Yesu Kristo na Mitume wake tujitie katika kuomba, kabla ya kumkubali na kumtuma mtu huyu, aliyeletwa kwetu kwa kazi ile ambayo twatumaini kwamba Roho Mtakatifu amemwitia.
Kisha isomwe Litania ya Kuamuru Wahudumu (Itaongozwa na Baba Askofu Sadock Makaya wa Western Tanganyika)
Kiongozi: Ee Mungu Baba wa Mbinguni:
Wote: Uturehemu maskini wenye dhambi
Ee Mungu mwana Mkombozi wa ulimwengu Uturehemu maskini wenye dhambi
Ee Mungu Roho Mtakatifu utokaye kwa Baba kupitia kwa Mwana.
Uturehemu maskini wenye dhambi
Ee Utatu Mtakatifu, Mtukufu, Nafsi tatu Mungu mmoja
Uturehemu maskini wenye dhambi
Ee Kanisa lako Takatifu Katholiko, lijazwe nawe kweli na upendo na lionekane bila mawaa siku ya kuja kwako.
Utusikie Bwana mwema
Kwa wateule wale wa Kanisa lako, ili watafute na kuona wito wao na huduma zao halisi.
Utusikie Bwana mwema
Kwa Jacob Askofu wetu Mkuu, na Maaskofu wote, Makasisi na Mashemasi, waone njaa ya kweli na kiu ya haki na kujazwa upendo wako.
Utusikie Bwana mwema
Askofu Mkuu amwombee atakayewekwa wakfu na familia yake:
Kwa huyu mtumishi wako Johnson Chinyong’ole atakayeamriwa kuwa Askofu leo, alitumikie Kanisa lako na kuonyesha utukufu wako ulimwenguni.
Utusikie Bwana mwema
Kwa nyumba yake na familia yake ipambwe na maisha safi ya Kikristo
Utusikie Bwana mwema
Kiongozi aendelee:
Kwa wale wote wanaolipenda na kulicha Jina lako Takatifu, wawe wamoja kama wewe ulivyo mmoja.
Utusikie Bwana mwema.
Kwa wale wasioamini, kwa wale waliopoteza imani yao, wapokee Nuru ya Injili.
Utusikie Bwana mwema.
Kwa mataifa yote ya ulimwengu, yaishi pamoja katika haki na amani.
Utusikie Bwana mwema
Kwa wote wenye mamlaka, wapende haki na kujenga heshima na uhuru wa kila mmoja.
Utusikie Bwana mwema
Kwa maskini na wanaoteswa, wagonjwa na wenye shida, kwa wafungwa wakimbizi na wale walio katika hatari, ili wafarijiwe na kulindwa
Utusikie Bwana mwema
Kwa upofu wote wa moyo, kiburi, majisifu na unafiki; kwa husuda, chuki na ukorofi na kutopendana kote.
Utuokoe Bwana
Kwa madanganyo yote ya dunia tamaa mbaya ya mwili na hila za shetani.
Utuokoe Bwana
Upende kutujalia toba la kweli; kutusamehe dhambi zetu zote na ulegevu na ujinga wetu; utukirimie neema ya Roho wako Mtakatifu, ili tutengeneze maisha yetu kwa Neno lako Takatifu.
Utusikie Bwana mwema
Bwana Uturehemu
Bwana Uturehemu
Kristo Uturehemu
Kristo Uturehemu
Bwana Uturehemu
Bwana Uturehemu
Baada ya Litania, Askofu Mkuu aseme sala ifuatayo:
TUOMBE
Mwenyezi Mungu mtoa mambo yote yaliyo mema uliyeamuru kwa Roho wako Mtakatifu daraja mbali mbali za Wahudumu wa Kanisa lako, umwangalie kwa rehema huyu mtumishi wako ambaye anaitwa sasa kwa kazi na huduma ya Askofu, umjaze kweli ya elimu yako umpambe maisha safi ili akutumikie amini kwa maneno na matendo yake katika daraja hili, jina lako litukuzwe na Kanisa lako lijengwe na kuongozwa vema. Kwa Bwana wetu Yesu Kristo Mwana wako aishiye na kumiliki, pamoja nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu Mungu daima, milele na milele. AMIN.
Kisha Askofu Mkuu, hali amekaa kitini pake, amhoji atakayewekwa wafu
Ndugu, kwa sababu Maandiko Matakatifu na taratibu za zamani zaamuru tusitie mikono kwa haraka, wala tusikubali mtu awaye yote awe na mamlaka katika Kanisa lake Kristo, alilolinunua kwa thamani kubwa ya kuimwaga damu yake; kabla sijakukaribisha kwa huduma hiyo, nitakuuliza mambo kadha wa kadha ili watu hawa waliopo, wapate kukupima, na kushuhudia, jinsi ulivyo na nia ya kuenenda katika Kanisa la Mungu.
Askofu Mkuu: Je, waamini sana kwamba umeitwa kwa kweli katika huduma hii, kama apendavyo Bwana wetu Yesu Kristo?
Askofu Mteule: Naamini hivyo
Askofu Mkuu: Je, waamini sana kwamba maandiko Matakatifu yanayo Elimu yote itoshayo na iliyofaradhi kwa wokovu wa milele kwa imani katika Yesu Kristo? Tena, umekusudia kabisa kuwaelimisha watu utakaokabidhiwa, katika Maandiko hayo Matakatifu, na kutofunza ya kuwa neno lolote na la faradhi kwa wokovu wa milele, ila yale ambayo utaona kwamba yanaweza kuthibitishwa na kuhakikishwa kwayo?
Askofu Mteule:Naamini, tena nimekusudia hivyo kwa Neema ya Mungu.
Askofu Mkuu: Basi, utasoma na kujifunza kwa uaminifu Maandiko hayo Matakatifu, na kumwomba Mungu akupe ufahamu wa kweli wa maandiko hayo; ili kwa hayo upate kufundisha na kuwaonya watu elimu yenye uzima, na kuwapinga wazushi na kuwahakikishia kweli?
Askofu Mteule: Nitatenda hivi, kwa msaada wa Mungu
Askofu Mkuu: Je, utakataa uovu wote na tamaa za dunia ukiishi maisha ya kiasi, na ya unyofu, na haki, katika ulimwengu huu, ujidhihirishe katika yote kuwa kilelelezo cha matendo mema kwa watu wengine, ili mshindani aaibishwe, asipate neno juu yako?
Askofu Mteule: Nitatenda hivyo, kwa msaada wa Bwana
Askofu Mkuu: Je, utahifadhi na kuongoza watu wote katika hali ya utulivu, na upendano na amani kwa kadri uwezavyo, na kuongeza hali hiyo. Na kwa mamlaka uliyonayo, kwa neno la Mungu utawarudi na kuwaadhibu wakorofi, waasi, na wenye hatia katika Dayosisi yako?
Askofu Mteule: Nitatenda hivyo kwa msaada waMungu
Askofu Mkuu: Utakuwa amini katika kuamuru, kutuma na kuwekea mikono wengine?
Askofu Mteule: Nitakuwa amini, kwa msaada wa Bwana.
Askofu Mkuu: Je, utahifadhi na kuongoza watu wote katika hali ya utulivu, na upendano na amani kwa kadri uwezavyo, na kuongeza hali hiyo. Na kwa mamlaka uliyonayo, kwa neno la Mungu utawarudi na kuwaadhibu wakorofi, waasi, na wenye hatia katika Dayosisi yako?
Askofu Mteule: Nitatenda hivyo kwa msaada wa Mungu
Askofu Mkuu: Utakuwa amini katika kuamuru, kutuma na kuwekea mikono wengine?
Askofu Mteule: Nitakuwa amini, kwa msaada wa Bwana
Askofu Mkuu: Kwa ajili ya Kristo, utakuwa mtu
mpole na mwenye Rehema, kwa maskini na wahitaji na wageni wote wasio na msaada?
Askofu Mteule: Ndivyo nitakavyokuwa, kwa msaada wa Mungu
Wote wasimame, kisha Askofu Mkuu naye asimame aseme:
Tuombe
Mwenyezi Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, aliyekupa nia njema ya kuyatenda haya yote akupe nguvu na uwezo uyatimize; akamilishe kwako kazi njema aliyoianza, ili uonekane mkamilifu bila lawama siku ya mwisho. Kwa Yesu Kristo Bwana wetu.
Wote: Amin
WIMBO: KWAYA
Kwaya inapoimba Askofu Mteule akavikwe mavazi yote ya Askofu isipokuwa Pete na Fimbo.
Askofu Mteule atakaporudi, Apige magoti mbele ya Askofu Mkuu.
WATU WAKAE.
Askofu Mkuu, Askofu Mteule na Maaskofu waliomleta wapige magoti.
Watu wote Waimbe. WIMBO wa Roho Mtakatifu:
Nyimbo Standard 210
- Ewe Roho wa Mbinguni
Uje kwetu sasa,
Ufanye makazi yako
Ndani ya kanisa.
- Ndiwe mwanga umulike
Tupate jikana;
Mengi kwetu yapunguka,
Tujalize Bwana.
- Ndiwe moto teketeza
Taka zetu zote;
Myoyo na iwe sadaka
Ya Mwokozi yote.
4. Roho wa Mbinguni uwe
Nasi hapa chini;
Mwili uufananishe
Na Kichwa Mbinguni
Kisha Askofu Mkuu asimame, na Maaskofu waliopo wasogee karibu naye, wengine upande wa mkono wake wa kulia na wengine upande wa kushoto.
Askofu Mkuu: Amani ya Bwana ikae nanyi daima
Wote: Pia na roho yako
Tuombe:
Mwenyezi Mungu, Baba mwenye Rehema nyingi, ambaye kwa wema usio na kiasi, ulimtoa mwana wako wa pekee umpendaye sana Yesu Kristo, awe Mkombozi wetu na mwanzo wa uzima wa milele; naye alipokwisha kukamilisha ukombozi wetu kwa kufa kwake, na kwa kupaa mbinguni, aliwakirimia watu karama zake nyingi, akifanya wengine, kuwa mitume, na wengine manabii, na wengine wainjilisti, na wengine wachungaji na waalimu, kwa ajili ya kulijenga na kulikamilisha Kanisa lake: Umpe twakusihi huyu mtumishi wako neema, awe tayari siku zote kuieneza Injili yako ndiyo furaha ya kupatanishwa nawe, ayatumie mamlaka aliyopewa, si kwa kuharibu, ila kwa kuokoa; si kwa kudhuru, bali kwa kusaidia; akiwapa watoto wako chakula kwa wakati wake, kama mtumishi mwaminifu mwenye akili akaribishwe mwisho katika furaha ya milele. Kwa Bwana wetu Yesu Kristo mwana wako, aishiye pamoja nawe katika Umoja wa Roho Mtakaifu, Mungu, daima milele na milele. Amin.
Watu waketi, kisha Askofu Mkuu akiwa ameketi, na Maaskofu waliopo wakiwa wamesimama, waweke mikono yao juu ya kichwa cha Askofu Mteule hali yeye amepiga magoti.
Askofu Mkuu aseme:
Pokea Roho Mtakatifu kwa daraja na kazi ya Askofu katika Kanisa la Mungu, unayokabidhiwa sasa kwa kuweka mikono yetu. Kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu. Amin.
Kumbuka kuichochea neema ya Mungu uliyopewa kwa kuwekewa mikono yetu. Kwa maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu, na ya upendo, na ya moyo wa kiasi.
Kisha Askofu Mkuu ampe Biblia, akisema.
Ufanye bidii, kuonya na kufundisha, uyatafakari mambo yaliyomo katika kitabu hiki. Uyasome kwa bidii ili faida itokanayo iwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako, na kudumu katika hayo maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.
Hapa ampe Pete ya Kiaskofu akisema:
Kwa watu na kundi la Kristo uwe Mchungaji, si Mbwamwitu.
Hapa ampe Fimbo ya Kiaskofu akisema.
Walishe usiwadhulumu. Wategemeze walio dhaifu, waponye wagonjwa, wagange waliopondeka moyo warudishe waliotupwa, watafute waliopotea. Uwe na rehema bali si kwa kuachilia mno; katika kuwarudi watu, usisahau rehema. Ili Mchungaji Mkuu atakapoonekana upokee taji ya utukufu isiyonyauka. Kwa Yesu Kristo Bwana wetu.
Wote: Amin
Maaskofu wengine wote watarudi kwenye viti vyao. Kisha Askofu wa Shinyanga atasimama na kurudi mahali pake na kuketi. Ndipo Askofu Mkuu naye arudi aketi mahali pake.
WIMBO: Nyimbo Standard 252. Kwaya ya Uvuke Iongoze.
NB: Beti tatu za kwanza zitaimbwa HALI WATU WAKIWA WAMEKETI.
- Nasikia Kwitwa
Na sauti yako
Nikasafiwe kwa damu
Ya kwangikwa kwako.
Nimesogea Mtini pako,
Unisafi kwa damu ya
Kwangikwa kwako.
- Ni mnyonge kweli,
Umenipa nguvu
Ulivyonisafi taka
Ni utimilivu.
- Yesu hunijuvya:
Mapenzi imani,
Tumai, amani, radhi,
Hapa na mbinguni.
Watu Wote wasimame wakati beti tatu za mwisho zinapoimbwa. (Maandalizi ya Sehemu ya Tatu ya Ibada yawe yanafanyika wakati huu, ikiwa ni pamoja na kuleta kiti cha Askofu Mkuu mbele ya Meza Takatifu).
- Huipa imara
Kazi yake ndani:
Huongezeka neema,
Ashindwe Shetani.
- Huishuhudia
Myoyo ya imani
Ya kuzipata ahadi
Wakikuamini.
- Napata wokovu
Wema na neema;
Kwako Bwana nina nguvu
Na haki daima.
Watu waketi.
SEHEMU YA TATU:
HUDUMA YA MEZA YA BWANA
SADAKA:
Zikusanywe wakati huu kwa muda mfupi kadri inavyowezekana. Wazee wa Kanisa wote wa Dayosisi ya Shinyanga waliopo wahusike.
KWAYA MBALIMBALI: Ziimbe wakati sadaka zinapokusanywa.
Wakati sadaka zikikusanywa Meza ya Bwana iandaliwe.
Sadaka zikiisha kukusanywa na kuletwa madhabahuni,
Askofu Mkuu aseme:
Askofu Mkuu: Ee Bwana, Ukuu, Nguvu, Heshima na Utukufu ni vyako, kwa kuwa vyote mbinguni na duniani ni vyako vitu vyote hutoka kwako na kwako tunakurudishia. Tunakuomba uzipokee na ubariki sadaka hizi na watu wako waliokutolea. Kwa Yesu Kristo Bwana wetu.
Wote: Amin
Amkio la Amani:
Askofu Mkuu: Amani ya B wana ikae nanyi daima
Wote: Pia na Roho yako
(Watu wapeane mikono kwa Amkio la Amani)
Askofu Mkuu: Bwana akae nanyi
Wote: Pia na Roho yako
Askofu Mkuu: Inueni mioyo yenu
Wote: Twainua kwa Bwana
Askofu Mkuu: Na tumshukuru Bwana Mungu wetu
Wote: Ni haki tena ni wajibu wetu
Askofu Mkuu: Ndiyo wajibu wetu, ni haki, tena ni faradhi na furaha kwetu, kila wakati na kila mahali tukushukuru Bwana Mtakatifu, Baba Mwenyezi, Mungu wa Milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Twakutukuza kwa ajili ya ulimwengu wote uliouumba na kuuhifadhi katika Yeye, kwa ajili ya taratibu za kuumba kwako na kwa ajili ya vipawa vyako vingi vya neema. Na zaidi ni wajibu wetu, sisi tulioanguka kukusifu kwa ajili ya upendo wako mkuu. Hata ukamtoa Mwana wako Yesu Kristo ambaye baada ya kufufuka kwake alipaa na kuketi kuumeni kwako na kama majira haya akawamwagia wana wako wateule Roho Mtakatifu kama alivyoahidi ili kuwafundisha na kuwaongoza katika kweli yote akiwapa ujasiri wa kuihubiri Injili kwa mataifa yote. Ee Baba twakusifu kwa ajili ya Roho wako Mtakatifu, ambaye anatufahamisha kwamba umetutia muhuri katika ubatizo, tuwe wako ili tupate kuyatangaza matendo yako ya ajabu. Kwa hiyo sisi nasi pamoja na malaika na manabii na mitume na mashahidi pia, na jeshi lote la mbinguni, twakutukuza na kukusifu daima tukisema:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Majeshi, Mbingu na nchi zimejaa utukufu wako: Utukufu una wewe Bwana uliye juu. Ndiwe Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Hosana palipo juu.
Wote Wakae
Askofu Mkuu Utukufu una wewe, Ee, Baba wa Mbinguni, ambaye kwa rehema zako kuu ulimtoa Mwana wako pekee Yesu Kristo ili wote wanaomwamini wawe na uzima wa milele. Utusikie, Ee Baba wa rehema tunakusihi, ili sisi, tukiupokea mkate huu na kikombe hiki, kama mwana wako alivyotuamuru, tuwe washiriki wa Mwili na Damu yake. Yeye usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru na kukutukuza, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema. Twaeni mle, huu ndio mwili wangu utolewao kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe akashukuru, akawapa akisema Nyweeni nyote katika hiki. Kwa maana hii ndiyo damu yangu ya Agano Jipya imwagikayo kwa ajili yenu na kwa ajili ya wengi. Kwa ondoleo la dhambi fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu.
Wote: Ee Baba, kufa kwake twakutangaza, kufufuka kwake twakukiri, kurudi kwake twakutazamia, utukufu una wewe Bwana.
Askofu Mkuu:
Kwa hiyo, Ee Baba, kwa mkate huu na kikombe hiki, tunafanya hivi kwa ukumbusho aliotuagiza Mwana wako, Yesu Kristo, tunaitangaza mauti yake iliyo dhabihu timilifu, aliyoitoa, msalabani kwa ajili yetu mara moja, na kuadhimisha ukombozi aliotupatia. Tunakushukuru, Ee baba, kwa ajili ya kufufuka kwake kwa uweza na kupaa kwake mbinguni, ambako anatuombea daima. Nasi twatazamia kurudi kwake kwa utukufu. Nawe utukubali katika yeye twakusihi tujazwe Roho wako Mtakatifu ili tuwe na Umoja katika Kanisa lako, ambalo unalikusanya kutoka pande zote za dunia, kwa yeye na ndani yake iwe kwako baba Mwenyezi katika Umoja wa Roho Mtakatifu, Heshima yote na Utukufu.
Wote: Baraka na shukrani na uweza zina Mungu wetu hata milele na milele. Amin.
Askofu Mkuu: Kama vile Bwana wetu Yesu Kristo alivyotuagiza akatufundisha tunathubutu kuomba.
Wote: Baba yetu, uliye mbinguni
Jina lako litukuzwe
Ufalme wako uje,
Mapenzi yako yatimizwe
Hapa duniani kama huko mbinguni
Utupe leo riziki yetu,
Utusamehe makosa yetu,
Kama sisi tunavyowasamehe waliotukosea,
Usitutie majaribuni
Lakini utuokoe na yule mwovu,
Kwa kuwa ufalme ni wako,
Na nguvu, na utukufu,
Hata milele, Amin
Wote:
Mwana Kondoo wa Mungu, uichukuaye dhambi ya ulimwengu uturehemu, Mwana Kondoo wa Mungu, uichukuaye dhambi ya ulimwengu, uturehemu, Mwana Kondoo wa Mungu uichukuaye dhambi ya ulimwengu, utupe amani yako.
Askofu Mkuu: Mkate tuumegao ni Ushirika wa Mwili wa Kristo.
Wote: Mkate ni mmoja, na sisi tulio wengi tu mwili mmoja kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.
Askofu mkuu: Bwana mwenye rehema
Wote: Hatustahili kuikaribia hii meza yako, kwa kuitegemea haki yetu wenyewe, Ila kwa rehema zako kuu na za ajabu, Hatustahili sisi kuokota makombo chini ya meza yako. Bali wewe ni Bwana yeye yule usiyebadilika, sifa yako ni kuwa na rehema daima. Kwa hiyo Bwana wa Neema, utujalie tuule mwili wa mwana wako mpendwa Yesu Kristo, na kuinywa damu yake, ili sisi wenye dhambi tusafishwe mwili na Roho tukaishi siku zote ndani yake na yeye ndani yetu. Amin.
Askofu Mkuu: Na tukaribie kwa imani, tuule mwili wa Bwana wetu Yesu Kristo alioutoa na kuinywa damu yake aliyoimwaga kwa ajili yetu. Tukumbuke ya kuwa alitufia sisi, tumpokee yeye mioyoni mwetu kwa imani na shukrani.
Mwili wa Kristo ukulindeni mwili na roho hata uzima wa milele.
Wote: Amin
Mhudumu: Damu ya Kristo ikulindeni mwili na roho hata uzima wa milele.
Watu: Amin
Askofu Mkuu atapokea Ushirika Mtakatifu na kumshirikisha Askofu wa Shinyanga. Maaskofu waliopo na Wahudumu watapokea Ushirika Mtakatifu. Watu watapokea Ushirika Mtakatifu kwa utaratibu uliopangwa. Utaratibu Utangazwe.
KWAYA MBALIMBALI
Ziwe zinaimba wakati wa Ushirika Mtakatifu.
Baada ya washiriki kupokea Ushirika Mtakatifu,
IBADA IENDELEE kama ifuatavyo.
Askofu Mkuu: TUMSHUKURU MUNGU
Kiongozi: Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana
Watu: Naam, vyote vilivyomo ndani yangu vilihimidi jina lake Takatifu.
Kiongozi: Ee nafsi yangu umhimidi Bwana
Watu: Wala usizisahau, fadhili zake zote
Kiongozi: Akusamehe maovu yako yote
Watu: Akuponya magonjwa yako yote
Kiongozi: Aukomboa uhai wako na kaburi
Watu: Akutia taji ya fadhili na rehema
Kiongozi: Aushibisha mema, uzee wako
Watu: Ujana wako ukarejezwa kama tai
Kiongozi: Utukufu una Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
Watu: Ulivyokuwa mwanzo, ulivyo sasa, na hata milele ni vivyo Amin.
Askofu Mkuu: Mwenyezi Mungu
Twakushukuru kwa kuwa
Umetulisha mwili wa mwana wako Yesu Kristo na damu yake; katika Yeye twakutolea nafsi zetu, roho zetu na miili yetu; Ututume kwa nguvu za Roho wako Mtakatifu, tuishi na kufanya kazi kwa sifa na utukufu wako. Amin.
Askofu Mkuu: Amani ya Bwana ikae nanyi daima.
Watu: Pia na Roho yako
Tuombe: Baba wa Rehema nyingi twakusihi umpelekee mtumishi wako Huyu Baraka yako ya mbinguni, umvike Roho wako Mtakatifu, ili yeye alihubiri Neno lako, awe na juhudi katika kurudi na kusihi na kukemea kwa saburi na elimu wala si hivyo tu bali awe kwao waaminio kielelezo cha kuwafaa katika Neno katika Usafi na Utakatifu. Aitimize Amini njia yake, aipokee siku ya mwisho Taji ya haki aliyowekewa na Bwana mhukumu mwenye haki. Aishiye na kumiliki pamoja nawe na Roho Mtakatifu Mungu mmoja milele na milele. Amin.
Ututangulie Ee Bwana katika matendo yetu yote kwa fadhili ya Neema yako, utuendeleze kwa msaada wa daima, ili kazi zetu zote zianzie kwako zikafulizwe na zikamalizikie kwako, tulitukuze Jina lako Takatifu, tukapate mwisho kwa Rehema yako Uzima wa Milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Amin.
SEHEMU YA NNE:
KUMWEKA KITINI ASKOFU WA PILI WA
DAYOSISI YA SHINYANGA
Ma-Canon wakiongozwa na Vicar General watakwenda alipo Askofu wa Shinyanga, Vicar General aliyeandaliwa kumweka kitini Askofu atamshika mkono wa kulia, na kumwongoza hadi penye Kiti chake cha Dayosisi:
NYIMBO STANDARD 534
- Bwana uliyewaita watakatifu wako,
Wawe mitume, wachunga walishe kundi lako,
Wanyonge na wenye hofu wakawa mashujaa,
Na wapole wa kunena wasiwe kunyamaa.
- Hata leo wawataka watakatifu wako,
Nawe wauliza tena ni nani aliyeko
Atakaye nimtume afundishe vijana?
“Ni tayari, Bwana wangu, Nitume mimi Bwana.”
- Nitume na mimi, Bwana, kama ulivyotumwa,
Habari ya Msamaha na dhambi kutubiwa,
Niwahubiri wakosa na waliopotea,
Wokofu wake Bwana, aliyewafilia.
- Astahiliye hapana kutamka habari,
Lakini wewe waweza kutufanya tayari,
Neno lako tulijue tupe na Roho yako,
Hayatakuwa ya bure hayo maneno yako.
Vicar General Canon James Tuli, hali amemshika Askofu mkono wa kulia atasema:
Bwana umwokoe mtumishi wako Johnson Japheth Chinyong’ole, Askofu wetu
Wote: Anayekutumaini
Kasisi: Bwana umletee msaada kutoka Patakatifu pako
Wote: Umlinde daima
Kasisi: Uwe ngome imara kwake
Wote: Usoni pa adui zake
Kasisi: Bwana Usikie sala zetu
Wote: Kilio chetu kikufikie
Kasisi aseme sala ifuatayo:
Baba wa Rehema zote, umjaze Roho Mtakatifu mtumishi wako Johnson Japheth Chinyong’ole ili atiliwe nguvu kwa kazi aliyokabidhiwa aifanye. Amin.
Ee Mwenyezi Mungu, ambaye kwa Mwana wako Yesu Kristo ulimjalia mtume wako Petro Mtakatifu vipawa vingi vilivyo bora ukamwamuru hasa kulisha kundi lako, twakusihi uwape Maaskofu wote na Wachungaji bidii na juhudi walihubiri Neno lako takatifu, na watu wako walifuate kwa utii, ili waipokee taji ya utukufu wa milele; katika Yesu Kristo Bwana wetu. Amin
Ndipo Kasisi aendelee:
Kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Amin
Mimi Kasisi Canon James Tuli, Kasisi Mkuu wa Shinyanga kwa Agizo la Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na kwa niaba ya Wahudumu na Wakrisito wote wa Dayosisi ya Shinyanga, nakupokea na kukukaribisha, Ee Baba Askofu Johnson Japheth Chinyong’ole, na kukuketisha katika Kiti cha Uaskofu huu wa Dayosisi ya Shinyanga katika Kanisa Anglikana Tanzania.
Bwana akuhifadhi kutoka kwako na kuingia kwako, tangu sasa hata milele.
Wote: Amin.
Kisha Kasisi Mkuu Canon James Tuli, hali akiwa upande wa kulia kwa Askofu, amwongoze Askofu wa Shinyanga kwenda mbele ya Watu. Wanapofika mbele ya watu, amshike Askofu mkono wake wa Kulia, na kusema:
Nawaleteeni, ninyi Makasisi, Mashemasi na Wakristo wote wa Dayosisi ya Shinyanga, Askofu wenu wa Kanuni, Baba Askofu Johnson Japheth Chinyong’ole, naye ndiye Baba yenu wa Kiroho. Mpokeeni.
Askofu arudi kuketi katika Kiti chake, Makasisi wa Dayosisi ya Shinyanga, wakianza Macanon, wasimame na kuapa mmoja mmoja. Baada ya kusoma kiapo, kila Kasisi/Mchungaji atapita kumshika Askofu mkono, na kurudi kuketi mahali pake.
Kiapo cha Makasisi:
Mimi........................................................naapa yamini yangu ya kuwa nitakutii wewe Johnson Japheth Chinyong’ole, Askofu wa Shinyanga, na Maaskofu watakaofuata, na kuzishika amri zako zilizo kanuni. Mwenyezi Mungu anisaidie.
Baada ya Makasisisi kuapa, Wakristo wote wa Dayosisi ya Shinyanga wasimame na kuapa kwa pamoja, wakiongozwa na wale walioandaliwa: mwanamume mmoja na mwanamke mmoja, waseme:
Kiapo cha Walei:
SISI Walei, wa Dayosisi ya Shinyanga, tunaahidi kukutii wewe, Johnson Japheth Chinyong’ole, Askofu wetu wa kanuni, na Baba yetu wa kiroho, kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Amin.
Kisha Makasisi na Mashemasi wa Dayosisi ya Shinyanga wasimame na Wakristo pia waendelee kusimama.
Askofu wa Shinyanga:
Mungu uwe kichwani mwangu na katika kufahamu kwangu;
Mungu uwe machoni mwangu na katika kutazama kwangu;
Mungu uwe ulimini mwangu na katika kusema kwangu;
Mungu uwe moyoni mwangu na katika kuwaza kwangu;
Mungu uwe nami wakati wa kufa kwangu na katika kuagana kwangu. Mungu awe pamoja nasi. Mungu awe katikati yetu.
Utukufu una Baba, na Mwana, Roho Mtakatifu.
Wote: Ulivyo kuwa mwanzo ulivyo sasa hata milele ni vivyo. Amin.
MWISHO:
Askofu wa Dayosisi ya Shinyanga atoe BARAKA
Amani ya Mungu ipitayo fahamu zote iwalindeni mioyo yenu na nia zenu katika hali ya kumjua na kumpenda Mungu, na Mwana wake Yesu Kristo Bwana wetu, na Baraka ya Mungu Mwenyezi Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, ikae nanyi sasa na hata milele. Amin.
Askofu: Bwana wetu Yesu Kristo alisema, kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi; Nendeni kwa amani.
Wote: Tumshukuru Mungu
WATU WAKAE.
Yafuate MATANGAZO NA SALAAM.
Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania asimamie sehemu hii, hasa muda.
1. Katibu Mkuu amwite MC wa Tafrija kutoa matangazo machache kuhusu mahali pa tafrija na utaratibu kwenda mahali hapo.
2. Katibu Mkuu awatambulishe kwa ufupi tu Maaskofu na baadhi ya wageni waliopo kuwataja majina tu na kuwaomba wasimame.
3. Askofu Mkuu na Mama Askofu Mkuu watoe salaam fupi kwa Kanisa Anglikana Tanzania kwa ufupi kwa Dayosisi ya Shinyanga.
4. Askofu wa Shinyanga atoe hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kutoa Salaam za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (dakika 10-15).
8. SALAAM ZA MGENI RASMI.
9. PICHA
NB: Watakaohusika katika picha na Mgeni Rasmi wajiandae mapema, na wawe karibu.
Baada ya kutoa Salaam za Serikali, Mgeni Rasmi ataombwa kupiga picha kama ifuatavyo:
- Mgeni Rasmi na Askofu Mkuu,
- Mgeni Rasmi na Askofu Mlezi
- Mgeni Rasmi na Baba na Mama Askofu Mlezi
- Mgeni Rasmi na Askofu Mstaafu na Mama wa Shinyanga.
- Mgeni Rasmi na Askofu wa Shinyanga,
- Mgeni Rasmi, Askofu wa Shinyanga, Mama Askofu wa Shinyanga na Watoto wa Askofu.
- Mgeni Rasmi, Askofu wa Shinyanga, Mama Askofu wa Shinyanga, na Wawakilishi wa Familia ya Askofu na Mama Askofu.
- Mgeni Rasmi, Askofu Mlezi, Askofu Mstaafu wa Shinyanga na Askofu wa Shinyanga
- Mgeni Rasmi, Askofu wa Shinyanga, Mama Askofu wa Shinyanga, na Askofu Mkuu, na Mama Askofu Mkuu
- Mgeni Rasmi na Maaskofu Waalikwa wa Madhehebu mbalimbali
- Mgeni Rasmi na Maaskofu Wote K.A.T,
- Mgeni Rasmi na Maaskofu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa na Wilaya
- Mgeni Rasmi na Maaskofu wastaafu
- Mgeni Rasmi na Askofu Mkuu , Askofu Mkuu Mstaafu, Dean, Waziri Mkuu Mstaafu, Katibu Mkuu na Askofu wa Shinyanga
BAADA YA PICHA
Baada ya Picha, Mgeni Rasmi atakwenda kupumzika. Atasindikizwa na Askofu wa Shinyanga pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania. Kisha Askofu wa Shinyanga na Askofu Mkuu watarudi kanisani kwa ajili ya Maandamano ya kutoka.
KUMALIZA IBADA
WIMBO WA KUTOKA
WIMBO: NYIMBO STANDARD 495
- Nimeahidi Yesu Kukutumikia,
Wewe U Bwana wangu, U Rafiki yangu;
Sitaogopa Vita, Wewe ndiwe Mweza;
Sitaiacha Njia, ukiniongoza.
- Dunia i karibu, Bwana siniache,
Na mengi majaribu yako pande zote;
Siku zote adui ni ndani na nje,
Bwana Yesu nivute, karibu na Wewe.
- Nikusikie Wewe, nena nami Bwana,
Kelele za dunia ndizo nyingi sana,
Nena kunihimiza, au kunionya,
Nena, nikusikie, Mwenye kuniponya.
- Umewapa ahadi wakufuatao,
Kwenda uliko Wewe wawe kuko nao;
Nami nimeahidi kukutumikia,
Nipe neema, Bwana, ya kukwandamia.
- Hatua zako Bwana na nizikanyage,
Wewe U mwenye nguvu, mimi ni mnyonge;
Niongoze, nivute, nishike daima,
Mwishoni niwasili mbinguni salama.
Utaratibu wa Kutoka Kanisani utakuwa kama ifuatavyo:
Watu Wote (walio ndani na nje ya jengo la Kanisa) wabaki hali wameketi mahali walipo.
Makasisi/Wachungaji, Mapdre wa Makanisa yaliyoalikwa watakuwa mbele, wakifuatwa na wale wa Kanisa Anglikana Tanzania, na ndipo wale wa Dayosisi ya Shinyanga. Kisha watafuata Maaskofu wa Madhehebu au Makanisa Mengine. Baada ya hapo watafuate Maaskofu Wastaafu wa Kanisa Anglikana. Ndipo wafuate Maaskofu wa Madayosisi katika Kanisa Anglikana Tanzania. Kisha Nyuma yao atasimama Chaplain wa Askofu wa Shinyanga, kisha Askofu wa Shinyanga, ndipo Msajili wa Kanisa Anglikana Tanzania, Kisha Chaplain wa Askofu Mkuu, ndipo Askofu Mkuu.
Muhimu: Maaskofu wakishatoka, watu wote wanahimizwa kuondoka katika eneo la Kanisa na kuelekea katika Ukumbi wa NSSF pasipo kuchelewa.
+++++MWISHO WA IBADA TAKATIFU++++++
HISTORIA YA MADAYOSISI YALIYOTANGULIA KUANZISHWA KWA DAYOSISI YA SHINYANGA
MAASKOFU WA DAYOSISI YA EASTERN EQUATORIAL AFRICA
- Askofu James Hannington 1884 – 1885
- Askofu Henry Perrot Parker 1886 – 1888
- Askofu Alfred Tucker 1890 – 1897
Maaskofu wa Dayosisi ya Mombasa kabla kuanzisha
Dayosisi ya Central Tanganyika 1899 - 1936
- Askofu William George Peel 1899- 1916
- Askofu Richard Stanley Heywood 1918 – 1936
Maaskofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika Kabla na baada ya kuanzishwa Dayosisi ya Victoria Nyanza 1927 –1963
- Askofu George Alexander Chambers 1927 – 1947
- Askofu William Wyn-Jones 1947 – 1950
- Askofu Alfred Stanway 1951 – 1971
- Askofu Yohana Madinda 1971 – 1989
- Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo 1989 – 2014
- Askofu Dkt. Dickson Daudi Chilongani 2014 -
Maaskofu wa Dayosisi Mama Victoria Nyanza kabla na baada ya kuanzishwa Dayosisi ya Shinyanga 1963 - 2017
- Askofu Maxwel Wigginis 1963 - 1976
- Askofu John Rusibamayila 1976 - 1991
- Askofu John Changae 1991 - 2008
- Askofu Boniface Kwangu 2008 - 2017
Maaskofu wa Dayosisi ya Shinyanga
- Askofu Charles Kija Ngusa 2005 - 2014
- Askofu Johnson Japhet Chinyong’ole 2018 -